tunajenga uchumi

huduma zetu ni kwa ajili yako

SEKTA ZETU

SUMAJKT INAFANYA KAZI KATIKA SEKTA NNE (4) AMBAZO NI;

01
SEKTA YA ujenzi
02
sekta ya viwanda
03
sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi
04
sekta ya biashara na huduma

mgawanyiko wa sekta zetu

1. sekta ya ujenzi

Jengo la Kitega uchumi la SUMAJKT lililopo eneo la Medeli, jijini Dodoma[/caption]

Mnamo, tarehe 24 Novemba 2018 Kampuni hii ilisajiliwa rasmi na BRELA kuwa kwa jina la SUMAJKT Construction Company Limited (SCCL).

Kampuni inatekeleza kazi za Ujenzi na Uhandisi kupitia kanda zake saba za Ujenzi ambazo ni:

  1. Kanda ya Mashariki (Dar es salaam, Pwani na Morogoro).
  2. Kanda ya Magharibi (Kigoma, Katavi na Tabora).
  3. Kanda ya Kati (Singida na Dodoma).
  4. Kanda ya Kusini (Mtwara, Lindi na Ruvuma).
  5. Kanda ya Kaskazini (Kilimanjaro, Tanga, Manyara na Arusha).
  6. Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe na Rukwa) na,
  7. Kanda ya Ziwa (Mwanza, Mara, Kagera, Shinyanga na Geita).

Kampuni ya umeme SECL ilianza ikiwa ni kitengo cha umeme ndani ya NSCD mwaka 2004 na kusajiliwa katika daraja la nne la ukandarasi wa umeme. 

Mwaka 2020 kitengo hiki kilipanda hadhi na kusajiliwa katika daraja la kwanza na Contractors Registration Board (CRB) ili kutekeleza kazi zote za usambazaji umeme na mifumo ya umeme. 

Mwaka 2021, SECL ilisajiliwa na BRELA kuwa kampuni ya SUMAJKT Electric Co. Ltd.

Kwa ujumla, sekta ya ujenzi imekuwa mstari wa mbele katika kufanikisha miradi mbalimbali ya ujenzi hapa nchini ikiwemo miradi ya kimkakati

Kampuni ya Huduma za Ushauri Elekezi katika Majenzi (SCBCL) ni kampuni mpya iliyotokana na uwepo wa wataalamu katika Idara ya Ujenzi NSCD waliokuwa wakijihusisha na usanifu, ukadiriaji majenzi na usimamizi wa miradi ya ujenzi.

Wazo la kuanzisha kampuni hii lilitokana na changamoto zilizokuwa zinajitokeza kwa vitengo vya Wasanifu (Architects), Wakadiriaji Majenzi (Quantity Surveyor) na Kampuni ya Uhandisi (Engineering Firms) kushindwa kuomba kazi za ushauri kupitia mwamvuli wa SUMAJKT CCL.

Kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Bodi za ERB na AQRB kampuni ya ukandarasi hairuhusiwi kufanya kazi za ushauri hivyo ikaonekana kuna haja ya kuanzisha kampuni inayojitegemea.

SCBCL ilipata usajili wa BRELA mnamo tarehe 21 Mei 2021 na kufanya mabadiliko ya majina ya vitengo mbalimbali ambavyo vimesajiliwa. Vitengo hivyo ni Wasanifu Majengo (Architects), Wakadiriaji Majengo (Quantity Surveyors) na Wahandisi Ushauri (Consulting Engineers).

Kampuni inaendelea kufanya kazi na kampuni nyingine na asasi mbalimbali za Serikali na watu binafsi.

Kampuni hii ilisajiliwa mwezi Novemba 2020, ambapo inajishughulisha na uzalishaji wa tofali aina zote (paving, cubestone, fensi louvers) na nguzo za uzio.

Ilianza kama mradi mnamo mwaka 1973 ikiwa ni kitengo cha ufundi ujenzi Makao Makuu Lugalo kwa kazi za kutengeneza tofali na kusaga kokoto.

Baadae ilihamishiwa JKT eneo la Kunduchi, jijini Dar es Salaam.

Mipango ya baadaye ni kusambaza bidhaa mbalimbali za ujenzi ikiwemo milango, madirisha ya chuma na bidhaa za ‘aluminium’ kwa wateja wanaoihitaji.

2. sekta ya viwanda

Kiwanda hiki kilinunuliwa na JKT tangu mwaka 1972 kama kiwanda kidogo cha kuzalisha samani kutoka kwa mmiliki binafsi aitwaye Luige na kukabidhiwa SUMAJKT mwaka 1982 kwa ajili ya mafunzo ya vijana na uzalishaji kibiashara.

Baada ya maboresho, kiwanda hiki kilisajiliwa mnamo tarehe 12 Machi 2020 kuwa kampuni kwa jina la “SUMAJKT Chang’ombe Furniture Co. Ltd”. Kiwanda kinachomilikiwa na Shirika kwa asilimia mia moja.

Lengo ni kutengeneza samani bora kwa ajili ya taasisi za Serikali, mashirika ya umma, makampuni na watu binafsi.

Kiwanda hiki kinachozalisha maji ya kunywa yanayoitwa “Uhuru Peak Pure Drinking Water”, kilianzishwa rasmi tarehe 17 Aprili 2018 kwa jina la SUMAJKT Bottling Plant. Kilisajiliwa kuwa Kampuni kwa jina la SUMAJKT Bottling Co. Ltd mwaka 2020.

Kiwanda kipo katika eneo la Mgulani JKT jijini Dar es Salaam. Kauli mbiu ya kiwanda ni “The Peak of Natural Purity”.

Wazo la uanzishwaji kiwanda cha maji lilikuja baada ya SUMAJKT kutaka kufufua kiwanda kilichokuwa cha dawa za binadamu cha TANZANSINO kwa kushirikiana na Umoja wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (TSSA). Tathimini ya kitaalamu ilifanywa kwa ushirikiano wa watendaji kutoka SUMAJKT, NHIF na MSD katika eneo la TANZANSINO na kushauri kuwa eneo halikidhi vigezo vya uanzishaji wa kiwanda cha kisasa cha dawa za binadamu.

Kwa kuzingatia ushauri huo Shirika liliamua kuanzisha kiwanda cha maji ya kunywa katika eneo hilo.

Maji yanayozalishwa na kiwanda hiki ni sehemu muhimu ya huduma ya maji ya kunywa safi na salama inayotolewa kwa jamii vikiwemo Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Taasisi za Serikali na watu binafsi katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Kiwanda cha bidhaa za ngozi SUMAJKT Leather Products kipo eneo la Mlalakuwa, jijini Dar es Salaam na kinajishughulisha na utengenezaji wa bidhaa za ngozi kwa ajili ya matumizi ya taasisi za ulinzi, shule, kampuni, pamoja na watu binafsi. Bidhaa zinazozalishwa ni pamoja na viatu, mikanda, mabegi na mikoba. Kiwanda hiki kilianzishwa rasmi tarehe 13 Julai 2017. Aidha, Kiwanda kilianza kwa kutumia moja ya majengo yaliyokuwa Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa Mlalakuwa Dar es Salaam na vyerehani vilivyokuwa vinatumiwa na Kampuni ya CAMISUMA kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa za ngozi. Kwa sasa kiwanda kimefanikiwa kununua vyerehani na mashine za kisasa za kutengeneza bidhaa za aina mbalimbali.

Hii ni kampuni ya Shirika inayojishughulisha na ushonaji wa mavazi ya aina mbalimbali kwa ajili ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama, makampuni na watu binafsi kilichopo Mgulani JKT jijini Dar es Salaam. Kiwanda kilianza uzalishaji rasmi tarehe 22 Aprili 2017 na kusajiliwa kuwa Kampuni ya Ushonaji SUMAJKT Garments Co. Ltd mnamo 27 Februari 2020. Kiwanda kimenunua mashine mpya na kuendelea kutumia majengo na baadhi ya mashine zilizoachwa na Kiwanda cha CAMISUMA kilichofungwa mwaka 2010.

Kampuni imekua mstari wa mbele katika kupunguza gharama za upatikanaji wa mavazi ya kijeshi kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la kujenga Taifa(JKT), Jeshi la Akiba (JA) na Jeshi la Uhifadhi (TFS, TANAPA, TAWA na NCAA). Taasisi mbalimbali, mashirika na watu binafsi wanapata huduma ya ushonaji mavazi katika kiwanda cha SUMAJKT Garments Co. Ltd.

Unga wa Mahindi kutoka Kiwandani kwetu SUMAJKT Mlale Food Processing

Hiki ni kiwanda cha Shirika kilichopo Mlale JKT Songea Mkoa wa Ruvuma. Kilianzishwa mwaka 2018 na kinajishughulisha na uchakataji wa nafaka za mahindi ili kuongeza thamani ya zao hilo kuleta manufaa ya kiuchumi kwa Shirika.

Kiwanda hiki kinazalisha unga unaoitwa “Mlale Sembe” ambao unasambazwa sehemu mbalimbali nchini.

Wazo la kuanzishwa kwa kiwanda cha Mlale lilitokana na hupatikanaji wa mahindi mkoa wa Ruvuma sambamba na mpango mkakati wa JKT kujitosheleza kwa chakula.

Kiwanda hiki kinazalisha unga bora wa mahindi kwa mahitaji ya Jeshi na jamii kwa ujumla.

Hii ni kampuni ya ubia kati ya SUMAJKT na kampuni ya ANIT ASFALT kutoka nchini Uturuki.

Shirika liliingia ubia na kampuni hiyo tarehe 07 Novemba 2015 kwa makubaliano ya kusaga na kuuza kokoto katika uwiano wa hisa 30% kwa SUMAJKT na 70% kwa ANIT ASFALT. Katika hisa hizo Shirika lilichangia kiasi cha fedha na kampuni ya ANIT ASFALT ilitoa mitambo.

Kampuni hiyo inaendelea na uzalishaji wa kokoto katika eneo la Pongwe Msungura Mkoani Pwani

3. sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi

Shughuli za uzalishaji kupitia kilimo zinaendeshwa kwenye maeneo mbalimbali ya Makambi na vikosi vya JKT. Kwa sasa, shughuli hizi husimamiwa na mameneja kwenye maeneo husika tofauti na hapo awali ambapo makamanda vikosi walikuwa wakisimamia shughuli hizo.

Shirika linaendelea kupanua shughuli za kilimo kwa kutafuta mashamba mapya na yale yanayotolewa na Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR) kwa lengo la kuyaendeleza kibiashara. 

Pia, Shirika linazalisha mazao mbalimbali kama vile alizeti na maharage katika shamba lake lililopo Hanang mkoani Manyara

4. sekta ya biashara na huduma

Hii ni Kampuni tanzu ya Shirika yenye Makao Makuu yake Mwenge, jijini Dar es Salaam. Kampuni inatoa huduma za kibiashara kwa kukodisha kumbi za sherehe, vyakula na mapambo katika matukio mbalimbali ya kiserikali na kijamii. Kampuni ilianza kama mradi mwezi Julai 2017 ikijulikana kwa jina la SUMAJKT Recreation & Catering Services kabla ya kusajiliwa rasmi mnamo tarehe 25 Machi, 2020.

Kampuni inaendelea kuboresha huduma zake ili kuweza kutoa huduma maeneo mengine nje ya Dar es Salaam.

Hii ni kampuni yetu ya ulinzi yenye dhamana ya kulinda majengo, wageni maalum, waajiriwa na umma kwa ujumla. Kampuni hii ina vifaa vya kisasa na miundombinu maalum kwa ajili ya kufanya kazi ya ulinzi na kudhibiti uhalifu kwa kiwango cha hali a juu.

Hii ni kampuni ya Shirika iliyosajiliwa rasmi mwaka 2020 kwa lengo la kusimamia shughuli za upakiaji na upakuaji wa mizigo bandarini na kuhakikisha usalama wa bidhaa zinazoingia na kutoka nchini. mwaka 2017, ilianza kutoa huduma ya kuratibu na kusimamia wafanyakazi wa kutwa wanaoingia kufanya kazi ndani ya bandari ya Dar es Salaam. 

Mwaka 2019, mradi ulipewa kazi ya kutoa huduma hiyo katika bandari za Kigoma na Mwanza. Kwa sasa, imeingia makubaliano mapya ya kuratibu na kusimamia wafanyakazi katika bandari zote zilizopo chini ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ambazo ni bandari za Dar es Salaam, Mwanza, Tanga, Mtwara, Kigoma, Kyela, Kasanga, Bukoba na Kemondo.

Kampuni inaendelea kufanya kazi kwa weledi na uaminifu katika kutoa huduma na kujenga imani kwa watumiaji wa bandari zote nchini baada ya kuamini kuwa ni sehemu salama ya kupitishia mizigo yao.

Kampuni hii inajishughulisha na kazi za kukusanya ushuru (Levy Collection), ukusanyaji madeni (Debt Collection) na udalali wa minada (Auctioneers) baada ya kusajiliwa tarehe 11 Juni 2019. Makao Makuu yake yapo Mlalakuwa, jijini Dar es Salaam. Wateja wakubwa wa kampuni hii ni Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Taasisi mbalimbali za kifedha, mashirika madogo madogo ya kifedha na kampuni za biashara. 

Wazo la kuanzishwa SUMAJKT Auction Mart Co. Ltd lilitokana na Shirika kuwa na wateja ambao hawalipi madeni kwa wakati baada ya kupata huduma kutoka kampuni tanzu na hivyo kulazimika kuanzisha kampuni hii badala ya kuendelea kutumia kampuni binafsi kukusanya madeni. Mpaka sasa, kampuni imefanya kazi nyingi hasa kwenye ofisi za halmashauri za wilaya hapa nchini na mpango wa baadaye ni kuboresha huduma zake na kufikia maeneo mengine ya nchi.

Kampuni hii ilisajiliwa mnamo mwezi Disemba 2021 kutoa huduma ya uwakala wa forodha na usafirishaji wa mizigo kwa JWTZ, JKT, SUMAJKT, mashirika ya umma na watu binafsi kwa lengo la kukuza huduma zake kibiashara. Makao Makuu yake yapo Mgulani, jijini Dar es Salaam. Kampuni ilianza kufanya kazi kama mradi mwaka 2013 ikijulikana kwa jina la SUMAJKT Clearing and Forwarding kwa lengo la kurahisisha uondoshaji na usafirishaji mizigo ya JWTZ na JKT (Inhouse Clearing and Forwarding).

Malengo ya baadaye ni kuboresha na kukuza shughuli zake kwa kupata vifaa wezeshi kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake.

Jitegemee Sekondari ni shule ya wavulana na wasichana kuanzia
kidato cha kwanza hadi cha sita. Shule hii ni ya Kutwa Pamoja
na huduma ya malazi kwa wanafunzi wanaoishi mbali na shule,
pamoja na wale wenye mahitaji maalumu yanayotokana na
mazingira yao ya kifamilia yasiyotoa nafasi nzuri ya mwanafunzi
kujisomea.

Chimbuko la shule hii ni Sera ya Elimu ya Watu Wazima ambapo
mwaka 1974 ilisajiliwa kama Kituo cha Elimu ya Watu Wazima
kikitoa elimu ya sekondari kwa maafisa na askari. Kwa wakati huo,
Shule iliitwa Mgulani (JKT) Sekondari. Baada ya kuwa na ongezeko
kubwa la Maafisa na Askari waliopata elimu ya sekondari na
mahitaji ya wazazi, Sera ya elimu ndani ya Jeshi ilibadilishwa.
Kutokana na mabadiliko hayo mwaka 1985 shule ilisajiliwa kutoa
elimu ya sekondari kwa wanafunzi wote.

Mnamo mwaka 2019 shule ilikabidhiwa SUMAJKT ili kuiendesha
kibiashara.

Shule ya Sekondari Kawawa ilianzishwa mwaka 1994 kwa lengo
la kutoa elimu kwa maafisa, askari, familia za askari na raia
wa maeneo jirani na shule. Ujenzi ulianza mwezi Agosti 1992,
ukifanywa na maafisa, askari wa Kikosi cha Jeshi 841 Mafinga JKT.
Shule hii ipo ndani ya Kikosi cha jeshi 841 Mafinga.
Shule ni ya mchanganyiko (wasichana na wavulana) na hutoa
huduma ya bweni na kutwa kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza
hadi cha sita. Shule ilisajiliwa kwa mchepuo wa kilimo kwa kidato
cha kwanza hadi cha nne. Aidha, mwaka 2008 shule ilipata kibali
cha kuanzisha kidato cha tano na sita kwa tahasusi ya sanaa (HGK,
HGL na HKL). Pia, mwaka 2022 shule ilianzisha shule ya awali na
shule ya msingi (Kawawa JKT Pre & Primary School).

Mnamo tarehe 10 Novemba 2018 shule ilikabidhiwa SUMAJKT ili
kuiendesha kibiashara.

Kampuni hii ilianzishwa mwaka 2020 kwa lengo la kutoa huduma
mbalimbali za afya ikiwemo huduma za madawa, vifaa tiba na
vifaa vya maabara. Makao Makuu yake yapo Mwenge Jijini Dar es salaam.
Siku za usoni, kampuni inalenga kuboresha huduma zake kwa kujielekeza kwenye huduma za uchunguzi na tafiti za afya, kufungua viwanda vya dawa na maduka makubwa ya dawa za binadamu maeneo mbalimbali nchini pamoja na kusambaza dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya.

Wafanyakazi wa kampuni ya SUMAJKT Cleaning and Fumigation wakiwa kwenye mavazi yao ya kazi[/caption]

Kampuni ya Usafi na Unyunyiziaji Dawa za Wadudu (SUMAJKT Cleaning and Fumigation Co. Ltd) yenye makao makuu yake Mwenge, jijini Dar es Salaam.

Ilianzishwa kama kitengo cha usafi ndani ya SUMAJKT Guard Co. Ltd mwezi Septemba 2018 na kusajiliwa rasmi BRELA tarehe 14 Machi 2020.

Tangu kuanzishwa kwake imekuwa ikijishughulisha na majukumu yake ya msingi ya kutoa huduma ya usafi na unyunyizaji dawa katika maeneo mbalimbali na inafanya juhudi kukuza huduma zake ili kufikia maeneo mengine ya nchi.

Mradi upo eneo la Mwenge Jijini Dar es Salaam. Mradi huu ni matokeo ya juhudi za Serikali zilizofanywa katika kutekeleza mpango wa kuinua sekta ya kilimo kupitia kauli mbiu ya “Kilimo Kwanza” mwaka 2009 kutokana na juhudi za Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu.

Shirika katika mpango huo lilipewa jukumu la kupokea kutoka Serikalini na kusambaza matrekta na zana  za kilimo zilizonunuliwa kutoka nje. Hivyo, JKT kupitia Shirika lilianzisha mradi wa matrekta ili kutekeleza jukumu hilo la Serikali.

Mradi huu umekuwa msaada kwa wakulima tangu kuanzishwa
kwake kwani wengi wamefaidika kupitia huduma ya Matrekta na
zana zake. Aidha, huduma ya kusambaza matrekta, zana na vipuri
vyake umesaidia kuanzisha mradi wezeshi wa kuuza matrekta,
vipuri na zana za kilimo kwa njia ya fedha taslimu.

Matrekta na zana hizo ni; Matrekta ya New Holland na FARMTRAC, majembe
ya kulimia (Disc Plough), jembe la kuvunja udongo (Disc harrow),
pump za umwagiliaji (Irrigation water pump) na tela (Trailer).

shuhuda

watu wanasemaje kuhusu sumajkt?

Kwa kweli nyumbani kwangu sasa hivi pamependeza sana, nashukuru tangu nimeanza kutumia fenicha za SUMA JKT sihangaiki tena kuzirekebisha kwa sababu ubora wake unadumu sana.
Kokunasri
Mjasiriamali
Aisee bidhaa za ngozi kutoka SUMA JKT zinadumu bwana. Hapa nina begi la ngozi nalitumia kwenda ofisini sahivi, lakini nilinunuliwa na baba yangu miaka 10 iliyopita nikiwa bado ni ngali mwanafunzi.
Biumrah
Mwanasheria