|

SUMAJKT Electric Co Ltd kuwasha umeme vijiji 51 wilayani Kishapu, Shinyanga.

Zoezi la uzinduzi wa kuwasha umeme limefanyika Februari 17, 2023 wilayani Kishapu, katika Kijiji cha Itilima Shule ya Msingi Isunda, mkoani Shinyanga huku vijiji vitatu vikiwashiwa pia huduma ya umeme ambavyo ni Itilima, Ikonokelo na Ipeja. Mkandarasi SUMAJKT Electric Co Ltd ambaye anatekeleza mradi wa Nishati Vijijini (REA) awamu ya tatu mzunguko wa Pili wilayani Kishapu na Shinyanga, ameanzakusambaza huduma za umeme katika Vijiji, Kaya na Taasisi za Serikali.

Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude akizungumza wakati wa uzinduzi wa kuwasha umeme wilayani Kishapu kwa vijiji hivyo vitatu, amepongeza kasi ambayo SUMAJKT Electric Co Ltd wameanza nayo ya kusambaza umeme kwa wananchi na taasisi za Serikali, na kuwaomba waendelee na kasi hiyo hiyo ili kufikia Agosti mwaka huu vijiji vyote 51 wilayani humo viwe na huduma ya umeme.
“Shukrani SUMAJKT naomba muendelee na bidii ya kuunganisha umeme kwa wananchi na Taasisi za Serikali na ikifika Agosti vijiji vyote 51 wilayani Kishapu viwe na umeme na kuchochea maendeleo ya kiuchumi,” amesema Mkude.


“Tunampongeza Rais Samia kwa kutoa fedha na kutekelezwa miradi hii ya umeme vijijini ambacho kilikuwa kilio cha wananchi kwa muda mrefu lakini ndani ya utawala wake wa miaka miwili wananchi wa Kishapu wanapata umeme na leo tumewasha katika vijiji vitatu,” ameongeza Mkude.


Naye Meneja wa Shirika la ugavi wa umeme Tanzania mkoani Shinyanga (TANESCO) Mhandisi Leo Mwakatobe, amesema Shirika hilo litapeleka wataalam kwenye vijiji hivyo vilivyounganishiwa Nishati ya umeme ili kutoa elimu kwa wananchi na wajiunge kwa wingi kuunganishiwa huduma hiyo.


Meneja wa TANESCO wilayani Kishapu Mhandisi Elias Turnbull, amewaonya wananchi ambao tayari wana Nishati ya umeme kijijini kwao, wasije wakatumia vishoka kuunganisha umeme kwenye Kaya zao bali watumie wataalam kutoka TANESCO.


Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo, amesema amefurahishwa na kasi ya usambazaji umeme katika vijiji wilayani Kishapu, na kuwaomba wananchi wasihujumu mradi huo na kuiba miundombinu yake na kuiingiza hasara Serikali, huku akiwataka viongozi na Jeshi la Jadi Sungusungu kuhakikisha ulinzi unaimarika ili usifanyike wizi wowote wa vifaa.


Aidha, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya umeme kutoka SUMA JKT Major James Mhame, amesema kwa kasi waliyonayo ya kusambaza umeme vijijini wilayani Kishapu kwamba hadi kufikia Agosti mwaka huu vijiji vyote 51 vitakuwa na huduma ya Nishati ya umeme, pamoja na wilaya ya Shinyanga vijiji 50 ambapo huko kampuni ya SUMAJKT Electric Co Ltd tayari wameshawasha umeme
vijiji 10, Kishapu vijiji vitatu na wiki ijayo watawasha tena vijiji vingine.


“Kasi tuliyonayo ni nzuri tayari tumeshapokea nguzo za
umeme 400 na zinakuja tena zingine 6,000 tunamuahidi
Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan hatutamwangusha kwa
kutuamini sisi SUMAJKT na kutupatia kazi hii ya
kusambaza Nishati ya umeme vijijini na tutamaliza ndani
ya muda,”amesema Meja Mhame.


Mwenyekiti wa Kijiji cha Itilima Mkwaya Mwandu, amesema kupata huduma hiyo ya Nishati ya umeme Kijijini humo itachochea fursa za kiuchumi, na kuipongeza Serikali kwa kuanzisha mradi huo wa umeme wa REA vijijini.

Similar Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *