Brigedia Jenerali Petro Ngata apokelewa kwa furaha SUMAJKT

Brigedia Jenerali Petro Ngata apokelewa kwa Furaha SUMAJKT

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la kujenga Taifa Brigedia Jenerali Petro Ngata, amepokelewa kwa furaha na Kamati ya Utendaji ya SUMAJKT katika ukumbi wa Mikutano, Mlalakuwa jijini Dar es Salaam.

Brigedia Jenerali Ngata akipokelewa kwa mara ya kwanza tangu apandishwe cheo hicho kutoka cheo cha Kanali, alianza kukaribishwa kwa gwaride la heshima na baadae kupokelewa na kamati ya Utendaji ya SUMAJKT.

Akizungumza katika ukumbi wa mikutano Brigedia Jenerali Ngata ametoa shukrani za dhati kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob Mkunda, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa na Afisa Mtendaji Mkuu Meja Jenerali Rajab Mabele kwa kumuamini na kumpatia jukumu la kuendesha Shirika la Uzalishaji Mali katika nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji.

Aidha amewashukuru Wakurugenzi, wakuu wa Miradi na Watendaji wote wa shirika kuendelea kumpatia Ushirikiano katika kuhakikisha SUMAJKT linatekeleza majukumu yake kwa weledi..

Akitoa shukrani hizo Brigedia Jenerali Ngata amefafanua kuwa ubora wa kazi na huduma zinazotolewa kwenye jamii na SUMAJKT ni ushirikiano mzuri baina yake na watendaji wote wa shirika katika nafasi mbalimbali.

“Katika utekelezaji wa majukumu yangu, siwezi kufanya chochote peke yangu, ipo Miradi mingi kila mwaka inayotekelezwa na Kampuni ya Ujenzi sasa Mkurugenzi hawezi akawa kila mahali, kuna watendaji katika ngazi ya Makao Makuu ambao ndio washauri wangu wa karibu, na ushauri huo umeniwezesha kutoa maelekezo yaliyo sahihi katika miradi yetu na ndio maana tumeweza kufanya vizuri kama Shirika.” Alisema Brigedia Ngata.

Aidha BRIGEDIA Jenerali Ngata, amewapongeza Wakurugenzi, Wakuu wa Miradi na watendaji wote kwa jitihada wanazozionyesha katika kutimiza majukumu kwani Shirika limeendelea kukua na kujitangaza kila kukicha kutokana na weledi wa watendaji.

Akikimkaribisha katika kikao hicho cha kumpongeza Brigedia Jenerali Ngata, Mkuu wa shule ya Sekondari ya Jitegemee JKT, Kanali Robert Kessy, amesema mapokezi hayo yameambatana na furaha za watendaji za watendaji ambao wanajivunia mafanikio hayo.

“Afande tunakupongeza na tuna furaha sana kukuona katika cheo kipya cha Brigedia Jenerali hata nyuso za watendaji zinaakisi furaha itokayo ndani kwenye mioyo, si kingine bali ni baraka ya kupandishwa cheo kwako.” Alisema Kanali Kessy.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Viwanda SUMAJKT Luteni Kanali Leah Mtuma, kwa niaba ya Wakurugenzi wa Shirika amesema wataendelea ushirikiano katika kutimiza majukumu ili kulifanya shirika lizidi kusonga mbele zaidi.

Baada ya kikap hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano Makao Makuu ya SUMAJKT Mlalakuwa ilifuatiwa na hafla fupi iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Uhuru uliopo Mwenge Jijini Dar es Salaam.

Similar Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *